Ijumaa 25 Septemba 2026 - 10:30
Mapadre Waandamana Kupinga Mauaji ya Kimbari dhidi ya Watoto wa Palestina na Lebanon

Hawza/ Zaidi ya mapadre 100, wakiwa wamebeba majina ya takribani watoto 300 wa Palestina na Lebanon waliouawa na Israel, walipita katika mitaa ya Roma huku wakisali, maandamano ya mtandao wa “Mapadre dhidi ya Mauaji ya Kimbari” yalihitimishwa mbele ya makao makuu ya Kampuni ya Leonardo, huku kukiwa na wito wa amani, diplomasia na kukomeshwa vitendo vya vurugu.

Shirika la Habari la Hawza – Zaidi ya mapadre 100 kutoka nchi nane na maeneo mbalimbali ya Italia, Jumanne, Septemba 22, 2026 (31 Shahrivar 1405), walishiriki katika maandamano ya pili ya mtandao wa kimataifa wa “Mapadre dhidi ya Mauaji ya Kimbari” yaliyofanyika katika mitaa ya Roma. Mtandao huu ulianzishwa mwaka mmoja uliopita, hafla hiyo iliambatana na dua na nyimbo za kidini, na ilianza katika Kanisa la Santo Spirito huko Sassia, karibu na Vatican, na kumalizika mbele ya makao makuu ya Kampuni ya Leonardo katika eneo la Prati.

Katikati ya maandamano hayo kulikuwa na kitambaa cheupe kilichofanana na sanda, ambacho kiliandikwa majina ya takribani watoto 300 wa Palestina na Lebanon waliouliwa na utawala wa Tel Aviv unaotuhumiwa kwa mauaji ya kimbari, baada ya kutangazwa usitishaji mapigano mara mbili. Washiriki walikuwa wameshika matawi ya mizaituni mikononi mwao na kusali kwa lugha mbalimbali, miongoni mwa waliokuwa mstari wa mbele katika maandamano hayo walikuwa ni Monsinyo Giovanni Ricchiuti na Monsinyo Christian Carlassare.

Njia ya maandamano ilipita kutoka Mtaa wa Conciliazione hadi Piazza Pio XII, kisha ikaelekea katika mitaa ya Porta Angelica, Cola di Rienzo na eneo la Prati, katika njia hiyo, vituo kadhaa vilipangwa kwa ajili ya dua na tafakuri, moja ya vituo hivyo kilitengwa Al-Tayyiba, eneo lenye wakazi wengi Wakristo katika Ukingo wa Magharibi, ambapo uliimbwa wimbo uliotungwa mahsusi kwa ajili ya tukio hilo na Padre Javier Morlans, ambaye ni padre na mwanamuziki kutoka Hispania.

Waandaaji walieleza kwamba; uchaguzi wa makao makuu ya Kampuni ya Leonardo kuwa sehemu ya mwisho ya maandamano hayo ulihusishwa na suala la viwanda vya kijeshi na biashara ya silaha kwa manufaa ya Israel. Mwishoni mwa hafla hiyo, pia walirejea Ibara ya 1 na Ibara ya 11 za Katiba ya Italia, na kusisitiza umuhimu wa kukomesha mantiki ya vita na kuzipa kipaumbele njia za kidiplomasia na zisizo za kutumia nguvu.

Don Rito Maresca, mmoja wa wanachama wakuu wa mtandao huo, alisema katika mahojiano na Shirika la Habari la ANSA: “Lengo letu, kwanza kabisa, ni kuelimisha na kuhamasisha jumuiya za Kikristo.” Alifafanua kwamba harakati hii imeundwa kwa lengo la kuonesha mshikamano na watu walioathiriwa na migogoro, kupitia dua na uwepo wa hadhara.

Wakati wa maandamano hayo, baadhi ya mapadre pia walirejea matamshi ya Papa Leo XIV kuhusu “amani iliyopokonywa silaha na inayopokonya silaha”, huku wakikosoa ongezeko la matumizi na uzalishaji wa kijeshi. Monsinyo Giovanni Ricchiuti, ambaye ni rais wa Pax Christi Italia, alikosoa kuendelea uwekezaji katika silaha, huku washiriki wengine wakitoa wito wa kuongezwa juhudi za kidiplomasia ili kukomesha migogoro.

Mtandao wa “Mapadre dhidi ya Mauaji ya Kimbari” kwa sasa umetangaza kuwa una zaidi ya wanachama 2,500 katika zaidi ya nchi 60, wanaofanya shughuli za kulaani jinai za utawala wa Tel Aviv unaotuhumiwa kwa mauaji ya watoto.

Maandamano ya Roma yalikuwa maandamano ya pili yaliyoandaliwa na mtandao huu, waandaaji walieleza matumaini kwamba katika siku zijazo hakutakuwa na haja ya kuyarejea tena, na kwamba jinai na dhuluma zinazofanywa na Israel katika eneo hilo zitakoma.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha